NEWS
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji..
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya uwekezaji na mitaji ya umma, Naibu waziri wa Madini, Kaimu Mkurungezi Mtendaji wa STAMICO, Kaimu Meneja Mkuu wa STAMIGOLD wakiwa kwenye ziara katika Mgodi wa STAMIGOLD Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma imefanya ziara katika Mgodi wa Stamigold mnamo tarehe 13/ 09/ 2021, Biharamulo Kagera. Kamati hiyo iliongozana na viongozi mbalimbali kutoka Serikalini: Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Elisha Manya, Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo Bi. Kemilembe Lwota, Kaimu Mkurungezi Mtendaji na STAMICO Dkt. Venance Mwase, Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa STAMIGOLD Bw. AIi Saidi na Uongozi wa Mgodi. Lengo kubwa ni kufuatilia ufikishaji wa umeme katika Mgodi na shughuli nyingine za uzalishaji. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na mitaji ya Umma Mhe. Atupele Fredy Mwakibeta ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Busoke, ametoa muda wa miezi miwili kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufikisha umeme Mgodini ili kuweza kupunguza gharama za uzalishaji. “Mgodi umekuwa ukiingia hasara ya kununua mafuta ya dizeli kwa ajili ya kuendeshea mitambo wakati tunaweza kupunguza gharama hizo kama tukiwa na umeme Mgodini.” Alisema Mhe. Atupele Pia Mhe. Atupele ameitaka Wizara ya Madini ifuatilie na kuhakikisha wanakutana na Waziri wa Nishati mpya Mhe. January Makamba ili waweze kutimiza lengo la kufikisha umeme Mgodini kwa wakati. Aidha, Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi Bw. Ali Saidi alisema Mgodi ukiunganishwa na umeme wa gridi ya taifa, utapunguza gharama zaidi ya milioni 700 kwa mwezi ambapo ni sawa na Bilioni 8.4 kwa mwaka, ambazo zinapotea kwenye kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya uchenjuaji. Mha. Godfrey Lweyemamu Mratibu wa Uboreshaji wa Biashara, alisema umeme umechelewa kufika Mgodini kutokana na mabadiliko ya Substation yaliyofanywa na TANESCO walipofika na kugundua kuwa umeme unaohitajika mgodini ni mkubwa ukilinganisha na umeme wa majumbani. Naibu wa Wizara ya Madini Prof. Manya alitoa shukrani zake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa kuja kutembelea mradi na kuaidi kutekeleza magizo yaliyotolewa kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
- News
- Hits: 996