Ni desturi ya Mgodi wa STAMIGOLD kudumisha na kuendeleza mahusiano mazuri na jamii inayouzunguka kama inavyoakisiwa na kauli mbiu yake “Nchi yetu Jukumu letu” ndiyo sera moja wapo ya maendeleo iliyowekwa kwa Taifa letu la Tanzania kuhakikisha makampuni mbalimbali yanatekeleza sera hiyo ya MPANGO WA MAENDELEO KWA WAZAWA. Sera hii inatoa mwongozo na kuhakikisha makampuni yote yanakuwa kipaumbele kuunga jitihada za wazawa katika kujiletea maendeleo yao binafsi, jamii zao na taifa kwa ujumla.
Stamigold inatekeleza sera hii kwa kiasi kikubwa kwenye jamii kwa kufanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali kwa wajasiriamali wanaojitokeza, kwa mfano upande wa vyakula (manunuzi ya Ng’ombe, matunda, mbogamboga), hununuliwa katika vijiji vya karibu na mgodi.
Wajasiriamali kutoka masoko mbalimbali walilieleza gazeti la “Stami news” jinsi wanavyofaidika na Mgodi na changamoto wanazopitia.
“Mgodi wa Stamigold umeniwezesha kutanua biashara yangu ya viazi, kwa kupitia faida nimeweza kutimiza mahitaji ya familia yangu, kununua usafiri na kumalizia ujenzi wa nyumba yangu,” Bahati Ernest mfanyabiashara wa viazi soko Mjinga alisema. Aidha aliongezea kwa kusema, wanafaidika na Mgodi kwa kiasi kikubwa kwani mzigo humalizika haraka kutokana na Mgodi kununua bidhaa kwa wingi ukilinganisha na soko la kawaida la kijijini. “Changamoto tunazopata ni kuongezeka kwa gharama za bidhaa pale msimu unapobadilika na kusababisha kupata hasara muda mwingine.” Bahati alisema.
Kikundi cha wanawake kutoka kijiji cha Mavota, wilaya ya Biharamulo walisema kupitia kilimo cha mbogamboga wanasaidia familia zao bila kutegemea msaada kutoka kwa waume zao. Kwani wanaamini mwanamke akijishughulisha anaweza kuwa msaada mkubwa sana katika jamii inayomzunguka.