Kampuni Tanzu ya STAMIGOLD inatarajia kuongeza uzalishaji wa dhahabu kutoka wakia 13,099 zilizochimbwa hadi April 2015 na kufikia wakia 25,000 ifikapo Desemba 2015 baada ya kusaini mkataba mpya wa uchimbaji Dhahabu.
 
Hayo yamesemwa na Maneja Mkuu wa STAMIGOLD Mhandisi Denis Sebugwao, mara baada ya kusaini mkataba mpya wa uchimbaji dhahabu katika mgodi wa Biharamulo baina ya STAMIGOLD na Junior Construstion Company Limited, katika hafla iliyofanyika hivi karibuni katika ofisi za   STAMICO makao makuu, jijini Dar es Salaam.
 
Mha. Sebugwao amesema utekelezaji wa mkataba huo ambao ni wa mwaka mmoja utaanza tarehe 1 Juni 2015 na kukamilika tarehe 30 Mei 2016 kwa gharama ya jumla ya dola za kimarekani milioni 19,499,200 sawa na shilingi bilioni 38.
“Mkataba huu ni bora, unalinda maslahi ya pande zote na unaleta matumaini katika uzalishaji wa dhahabu kutokana na umahiri wa Kampuni ya Junior Construstion Company Limited katika kutumia mitambo ya kisasa ya uchimbaji madini na watalaam waliobobea katika fani hiyo” Alifafanua Mha. Sebugwao.
 
Aidha amesema, mkataba huo pia unaitaka Kampuni hiyo kufanya kazi ya uchimbaji kwa kuzingatia Sheria ya Madini Na. 14 ya 2010; Sera ya Taifa ya Madini ya mwaka 2009; taratibu za uendeshaji migodi; umiliki wa leseni za mitambo ya uchimbaji madini; na sheria za hifadhi ya mazingira, afya na usalama wa wafanyakazi na mgodi kwa ujumla.
 
“Jambo jingine la kujivunia katika mkataba huo ni kwamba Kampuni ya Junior Construstion Company Limited itaendesha mitambo yake huku ikigharamia mafuta kwa ajili ya uendeshaji wa mitambo hiyo jambo ambalo linatuletea unafuu mkubwa katika kudhibiti gharama za uzalishaji wa dhahabu tofauti na mkataba uliopita” Aliongeza Mha. Sebugwao.
 
Kampuni ya STAMIGOLD iliamua kutangaza zabuni ya kazi hiyo ya uchimbaji madini katika mgodi wa Biharamulo mwezi Desemba 2014 baada ya Kampuni ya KASSCO iliyokuwa ikifanya kazi hiyo kukamilisha mkataba wake.
Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Junior Construstion Company Limited Bw. Suleiman Masoud Suleiman ameihakikishia STAMIGOLD kuwa Kampuni yake itafanya kazi hiyo ya uchimbaji kwa kutumia mitambo mipya na ya kisasa itakayoinua kiwango cha ufanisi na kuwezesha kazi kukamilishwa kwa muda uliopangwa.
 
Bw. Suleiman ameiomba STAMIGOLD kuipa ushirikiano Kampuni yake katika kutekeleza mkataba huo, na kusikilizana nao pale itakapotokea tofauti, ili kutimiza malengo ya Serikali kwa pamoja na kuisaidia Serikali kuongeza imani kwa Kampuni za Kizalendo katika kutekeleza kazi mbalimbali.
 
Ameishuruku STAMIGOLD na Serikali kwa kutambua mchango wa Kampuni za Kizalendo katika kukuza uchumi,  kupanua soko la ajira kwa Watanzania, kufanya kazi kwa uweledi na kutumia teknolojia ya kisasa katika kuongeza ufanisi wa kazi.
 
Akifafanua kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Mhandisi Edwin Ngonyani amesema anaridhika na utendaji bora wa STAMIGOLD, Kampuni tanzu ya kwanza ya STAMICO, na kwamba Shirika litaendelea kutekeleza miradi yake kupitia Kampuni Tanzu mbalimbali ili kukuza soko la ajira, kuimarisha uwezo katika uchimbaji madini na kukuza biashara ya madini kwa manufaa ya watanzania na Taifa kwa ujumla.
 
Mha. Ngonyani amesema ndoto yake ni kuona STAMICO inachangia kwa kiwango kikubwa katika azma ya Serikali ya kuongeza ajira kwa wasomi nchini na mapato kwa Mfuko Mkuu wa Hazina na hivyo kupaa kwenye wingu la mafanikio katika kipindi cha miaka miwili tu ijayo. Katika kipindi hicho cha miaka miwili, STAMICO itaweza kujitegemea na kuanza kupeleka fedha Hazina na hivyo kuacha kabisa kutegemea fedha za ruzuku kutoka Serikalini.
 
Ameitaja miradi mingine ni pamoja na mradi wa Ununuzi wa Madini ya Bati Kyerwa mkoani Kagera unaotekelezwa na kampuni tanzu ya Kyerwa Tin Company Limited; Mradi wa uchimbaji makaa ya mawe Kiwira na uzalishaji wa umeme wilayani Ileje unaotarajiwa kutekelezwa kwa ubia kuanzia mwaka 2016; na Mradi wa uchimbaji na uchenjuaji dhahabu wa Buhemba wilayani Butiama ambao unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka ujao wa fedha baada ya kukamilisha hatua za kumpata mbia kwa njia ya zabuni.

Connect with us

Stamigold Company Limited, Plot # 417/418, United Nations Road, Upanga, Dar es salaam

  • +255 (22) 2151717/3
  • info@stamigold.co.tz

 

Newsletter

Enter your email address

Search