Wachimbaji Nemba

Kikundi cha wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Nemba Group kutoka kijiji cha Nemba  wilaya ya Biharamulo wameaswa kufanya shughuli zao kwa uwazi na ukweli huku wakizingatia sheria ili kuwa na uchimbaji madini wenye tija kwao na taifa.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na aliyekuwa akikaimu nafasi ya Meneja Mkuu wa mgodi wa Biharamulo, Korodias Shoo wakati wa kikao baina yake na kikundi hicho kilichofika hapa mgodini.

Shoo alisema ni vyema kikundi kufanya kazi zake kwa uwazi na ukweli na kuepuka kudanganya kile kinachoendelea katika shughuli zao kwani hata Serikali inapenda kuona wachimbaji wadogo wanakuwa na uchimbaji endelevu ambao utawatoa kwenye uchimbaji mdogo na kuwafikisha kwenye uchimbaji wa kati.

“Ningependa kushauri kikundi chenu kiwe wazi hususani kwa viongozi katika kila hatua mnayopitia katika  shughuli zenu na hasa kuepuka kudanganya  kinachoendelea katika uchimbaji hii itawasaidia hata pale mnapokwama waweze kufahamu ni kwa namna gani wanaweza kuwasaidia na hii itawezekana ikiwa mtafanya shughuli zenu kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa katika sekta ya uchimbaji madini” Alisema Shoo

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Sylivester Kisusi alibainisha kuwa tayari kikundi kimeanza uchimbaji lakini uzalishaji haujaanza kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa vifaa vya uchimbaji na uchorongaji ambapo Kaimu Meneja Mkuu wa mgodi aliwaeleza kuwa Wizara ya Nishati na Madini hutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo kwa kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) hivyo ni vyema kufuatilia suala hilo zaidi kwa  Afisa madini mkoa ili kufahamu vigezo vya kupata ruzuku.

Kisusi aliongeza kuwa changamoto zingine zinazowakabili ni pamoja na uhaba wa fedha, uhaba wa baruti za uchimbaji, vifaa vya kuhifadhi maji, ukosefu wa barabara ya kuelekea eneo lao la uchimbaji na ukosefu wa vifaa vya kujikinga kazini (PPE) kwa wachimbaji na kuomba uongozi wa mgodi kusaidia kuzitatua pamoja na kuwapatia wataalam wa kutembelea mgodi wao ili kutoa ushauri wa kitaalam hususani matumizi sahihi ya baruti za uchimbaji.

Katika hatua nyingine, Shoo alibainisha kuwa suala la mgodi kuwepo ndani ya hifadhi ya misitu inalazimu shughuli zote zitakazofanyika kupata kwanza kibali kutoka kwa wakala wa misitu  hivyo ni vigumu kwa mgodi wa Biharamulo kuwasaidia kutengeneza barabara ya kuelekea eneo lao la uchimbaji. Vilevile ombi la kikundi  kupatiwa madumu ya kuhifadhi maji na wataalam wa masuala ya uchimbaji kutoka mgodi lilikubaliwa.

 Aidha, Katibu wa kikundi cha Nemba, Masanja Maduhu alihitimisha kwa niaba ya kikundi kwa kuuomba uongozi wa mgodi kuendelea kutoa ushauri kwa kikundi kila unapohitajika pamoja na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili ikiwa zipo ndani ya uwezo wao.

“Kwa niaba ya wenzangu ningependa kuushukuru uongozi wa mgodi kwa ukarimu wao na hasa maelekezo ya namna tunavyoweza kutatua baadhi ya changamoto zinazotukabili pamoja na ahadi ya kupatiwa wataalam watakaotembelea eneo letu la uchimbaji kutushauri ili na sisi kama wazawa tuwekeze kwenye rasilimali za taifa kwa faida. Tunaomba mgodi usichoke kutusaidia pale tunapokwama hata pale tutakapo hitaji ulinzi wa ziada tunaomba kusaidiwa hilo pia ” Alisema Maduhu.
W
Mgodi wa Biharamulo tangu kuanzishwa kwake umekuwa ukisaidia vikundi mbalimbali vya wachimbaji wadogo wa madini wanaofanya shughuli zao katika maeneo tofauti ndani ya wilaya ya Biharamulo ikiwa ni sanjari na kutekeleza wito uliotolewa na serikali wa kuhakikisha migodi inasadia vikundi vidogo vinavyotaka kujihusisha na uchimbaji wa madini ili kupunguza migogoro sehemu za uchimbaji na vile vile kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira na hasa kwa vijana.
 

Connect with us

Stamigold Company Limited, Plot # 417/418, United Nations Road, Upanga, Dar es salaam

  • +255 (22) 2151717/3
  • info@stamigold.co.tz

 

Newsletter

Enter your email address

Search